Tuesday, April 9, 2013

Uhuru Kenyatta aapishwa kuwa rais Kenya


Uhuru Kenyatta aapishwa kuwa rais Kenya

Nairobi Kenya -  09/04/2013. Uhuru Kenyatta ameapishwa kuwa rais wa nne wa Kenya. Viongozi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika wameudhuria kuungana na Wakenya kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais  huyo mpya wa Kenya kwenye uwanja wa mpira wa Kasarani.
Kenyatta mwenye umri wa miaka 51 ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta. Ushindi wake wa asilimia 50.07 katika uchaguzi wa tarehe 4 Machi ulihalalishwa na Mahakama ya Juu baada ya pingamizi lililowekwa na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Raila Odinga, kutupiliwa mbali na mahakama hiyo.

Kenyatta anayekuwa rais wa nne wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki tangu lilipopata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1963, anakuwa rais wa pili barani Afrika kuwa madarakani hali anakabiliwa na mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za kusaidia kuchochea ghasia za kikabila zilizoukumba uchaguzi wa urais wa Kenya wa mwaka 2007. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mwezi Julai, ambapo Kenyatta na naibu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya aina moja.

Mtaalamu wa masuala ya Kenya katika Chuo Kikuu cha Warwick, Daniel Branch, amesema "mataifa ya Magharibi yamejikuta kwenye hali ngumu sana, lakini huenda kila nchi ikatafuta njia yake yenyewe na mahusiano na Kenya.
Hata hivyo rais Uhuru Kenyatta amehaidi kushirikiana na yote yanayo husu maswala ya kimataifa atayafuatilia na kuyatekeleza.








Monday, April 8, 2013

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza aaga dunia.

Margaret Thatcher  aaga dunia

London Uingereza - 08/ 04/ 2013Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Margaret Thatcher ambaye alikuwa akijulikana kama "Iron Lady" kwa ukakamavu wake ambaye amezifanyia marekebisho siasa za kizazi cha Uingereza amefariki dunia baada ya kupigwa na kiharusi leo akiwa na umri wa miaka 87. Mengi zaidi na Mohammed Dahman.
Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza na Waziri Mkuu David Cameron wameongoza katika salamu za rambi rambi kwa waziri mkuu huyo wa kwanza mwanamke nchini Uingereza, muumini mashuhuri kabisa wa sera za mrengo wa kulia na mtu muhimu wakati wa Vita Baridi.
Msemaji wa familia ya Thatcher amekaririwa akisema "kwa masikitiko makubwa Mark na Carol Thatcher (watoto wa marehemu) wanatangaza kwamba mama yao Bi. Thatcher amefariki kwa utulivu baada ya kupigwa na kiharusi leo asubuhi."

Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye aliiongoza Uingereza kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 1990 alikuwa akikabiliwa na maradhi ya kupoteza kumbukumbu na mara chache amekuwa akionekana hadharani katika miaka ya hivi karibuni.

Mara ya mwisho alilazwa hospitalini hapo mwezi wa Disemba mwaka jana kwa ajili ya operesheni ndogo ya kuondowa uvimbe kwenye nyonga yake.
Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Conservative amebakia kuwa waziri mkuu pekee mwanamke katika historia ya Uingereza na kiongozi aliekaa mfululizo kwa muda mrefu kabisa katika makao makuu ya serikali ya Downing Street katika karne ya 20.
Binti yake wakati fulani aliwahi kusema kwamba waziri mkuu huyo wa zamani inabidi akumbushwe mara kwa mara kwamba mume wake Denis amefariki mwaka 2003.
Thatcher alitakiwa na madaktari kuacha kuhutubia hadharani muongo mmoja uliopita baada ya kukumbwa mara kadhaa na kiharusi kidogo.

Kasri la Kifalme la Uingereza Buckingham Palace limetowa taarifa ikisema kwamba Malkia amesikitishwa kusikia habari za kifo cha Thatcher na kwamba atatuma ujumbe binafsi wa masikitiko kwa familia.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amekatisha ziara yake katika nchi kadhaa za Ulaya na amesema kwamba kwa huzuni kubwa amepokea habari za kifo cha Bibie huyo na kwamba wamempoteza kiongozi adhimu,waziri mkuu adhimu na Muingereza adhimu.Ameongeza kusema kwamba Thatcher " ameitumikia nchi yake vizuri sana,ameiokoa nchi yake na ameonyesha ushujaa mkubwa sana katika kufanya hivyo.Watu watakuwa wanajifunza juu ya kile alichokifanya na mafanikio yake kwa miongo kadhaa inayokuja na yumkini hata kwa karne kadhaa.Hiyo dio haiba yake.”

Michael Howard kiongozi wa chama cha Conservative kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2005 amekiambia kituo cha televisheni cha Sky kwamba ni habari za kuhuzunisha sana kwani alikuwa ni mashuhuri sana katika siasa za Uingereza.

Howard anaamini kwamba Thatcher ameiokoa nchi yao, ameubadili uchumi wa nchi hiyo na anaamini kwamba ataingia katika historia akiwa kama mmojwapo wa mawaziri wao wakuu walio adhimu kabisa.

Wafuasi wa sera za mrengo wa kulia wanampongeza mama huyo kwa kuitowa Uingereza kwenye msononeko wa kiuchumi lakini wafuasi wa mrengo wa shoto wanamshutumu kwa kuving'owa viwanda vilivyokuwepo tokea enzi za jadi na kuvunja kiini cha mshikamano wa jamii.

Katika jukwaa la kimataifa alijenga uhusiano maalum na Rais Ronald Reagan wa Marekani jambo ambalo limesaidia kuuangusha ukomunisti katika Muungano wa Kisovieti.Pia alikuwa akipinga vikali uhusiano wa karibu wa Ulaya.

Thatcher alizaliwa akiwa anajulikana kwa jina la Margaret Hilda Roberts hapo tarehe 13 Oktoba mwaka 1925 katika mji wa sokoni wa Grantham mashariki ya Uingereza akiwa ni binti wa muuza duka la vyakula na bidhaa ndogo ndogo.

Baada ya kumaliza shule na kujipatia shahada yake ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Oxford alifunga ndoa na mfanyabiashara Denis hapo mwaka 1951 na miaka miwili baade walibarikiwa watoto mapacha Carol na Mark. Mara ya kwanza alichaguliwa katika bunge hapo mwaka 1959 na alichukuwa nafasi ya waziri mkuu wa zamani Edward Heath kama kiongozi wa chama cha upinzani cha Conservative hapo mwaka 1975 kabla ya kuwa waziri mkuu miaka minne baadae.

Haiba yake ya kudumu inaweza kuelezwa kwa muhtasari kuwa ya "Thatcherism " yaani mkusanyiko wa sera ambapo wafuasi wake wanasema zimeendeleza uhuru wa mtu binafsi na kusambaratisha mgawanyiko wa kitabaka ambao ulikuwa umeipasuwa Uingereza kwa karne kadhaa.

Hata hivyo kushinikiza sera zake kuliiweka serikali yake katika mapambano kadhaa magumu.Itakumbukwa wakati Argentina ilipovivamia visiwa vya Falklands vilivyoko chini ya himaya ya Uingereza hapo mwaka 1982, Thatcher alituma vikosi na meli za kivita na kuvikombowa katika kipindi cha miezi miwili.
Na hadi sasa visiwa kisiwa cha Falklands kimekuwa na mzozo kati ya Argentina na Uingereza nani ni mmiliki halali wa ene hilo.



Tuesday, April 2, 2013

Wavenezuela kuchagua upya baada ya Chavez.

Karaca , Venezula - 02/04/2013. Viongozi wa wanao gombania kuwania kiti cha urai wa Venezuela kilicho achwa wazi na hayati Hugo Chavez wameanza kampeni za uchaguzi ili kuongoza nchi yao.
Nikolas Maduro ambaye nimgombea wa chama tawala na aliye pewa baraka na Hugo Chavez kugombe kiti cha urais kabla ya kifo chake, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu kumpiku kiongozi wa chama cha upinzani Henrique Kapriles ambaye alishindwa Hugo Chavez  wakati wa uchaguzi wa kwanza wa urais. Tangu kifo cha Hugo Chavez kumekuwa na maoni tofuti juu ya nani atashinda kiti hicho cha urais nchini Venezuela.

Korea ya Kaskazini ya zidi kuwa kichwa ngumu.

 Pyongyang, Korea ya Kaskazini - 02-03-2013. Serikali ya Korea ya Kaskazini imetangaza kufungua kinu chake cha kinyuklia ambacho ilikuwa imekifunga hapo awali.
Kwa mujibu wa habari kutoka serikali ya Korea ya Kaskazini zinasema " tunaamua kufungua kinu hicho  kwani kitawasaidia katika miradi ya umeme."
Uamuzi wa huo wa Korea ya kaskazini kufungua kinu hicho walichokifunga mwaka 2007, umekuja huku kuna hali kutishiana kivita kati yake na Korea ya Kusini.
Hata hivyo Korea ya Kusini imesema ikiwa itashambuliwa na Korea ya Kaskazini itajibu mashambulizi hayo.